Katika miaka ya hivi karibuni, inaonekana kwamba kiwango cha heroini kilichokuwa kikisafirishwa kutoka Afganistani kupitia kwa mtandao wa njia za baharini Afrika Mashariki na Kusini kimeongezeka sana. Soko jumuishi la uhalifu linalokuza na linalokuzwa na matukio ya kisiasa katika ukanda huu, limejitokeza. Sasa hivi, Afrika inapitia kipindi cha ongezeko kubwa zaidi duniani kote la matumizi ya heroini, na aina mbalimbali za mitandao haramu na wanasiasa wa tabaka za juu wa Afrika Mashariki wamezama kabisa katika biashara hii. Sera yenye mikabala mipya inahitajika kwa dharura.
Kuhusu waandishi
Mark Shaw ndiye mkurugenzi wa Shirika la Dunia la Kupambana na Uhalifu wa Kupangwa Unaokiuka Mipaka ya Nchi (GIATOC) na pia ni mwanazuoni mwandamizi katika Mradi wa Kimataifa kuhusu Sera ya Madawa ya Kulevya katika Shule ya London ya Uchumi. Mpaka hivi karibuni amekuwa Profesa wa Haki na Usalama katika Kituo cha Elimu ya Jinai katika Chuo Kikuu cha Cape Town, anakofundisha. Amewahi kufanya kazi katika nyadhifa mbalimbali katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Madawa ya Kulevya na Uhalifu.
Peter Gastrow ni mshauri mkuu wa GIATOC. Anaishi Cape Town na amefanya kazi kama wakili wa Mahakama ya Upeo, ameshahudumu kama mbunge, na pia kama mshauri wa waziri wa polisi wa Afrika Kusini. Uhalifu wa kupangwa umekuwa swala analolizingatia katika utafiti wake tangu afanye kazi kama mkurugenzi wa Cape Town wa Taasisi ya Masomo ya Usalama, na mwanazuoni mwandamizi katika Taasisi ya Kimataifa ya Amani huko New York.
Simone Haysom ni mchanganuzi mwandamizi wa GIATOC na pia ni mwanazuoni anayetembelea Idara ya Masomo ya Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Oxford. Amewahi kufanya kazi kama mtafiti katika Taasisi ya Maendeleo ya Ng’ambo ya London, na amefanya kazi miaka mingi kama mtaalamu wa masuala yanayohusiana na uhamishwaji wa lazima kutoka kwa makazi, maendeleo ya miji, uhalifu wa kupangwa na kazi ya polisi.
Picha ya jalada: © Africa Studio – Adobe Stock