Kenya hupeleka wafanyakazi nje ya nchi hasa Mashariki ya Kati na kwa kiwango kidogo hadi Ulaya, Amerika ya Kaskazini na Afrika. Hata hivyo, Wakenya wengi wanazuiliwa kama watumwa katika nchi za Mashariki ya Kati. Wafanyabiashara haramu wanaweza kuendesha shughuli zao hasa kwa sababu ya hali mbaya ya kijamii na kiuchumi ya Wakenya na mapengo na upungufu katika ulinzi wa kisheria za wafanyakazi wahamaji.
Huku nchi ya Kenya ikiwa na sheria nyingi za kazi, zingine hazitumiki moja kwa moja katika usafirishaji wa wafanyakazi nje ya nchi na hivyo basi kuzifanya zisifae usalama wa wafanyakazi wahamaji. Pia kuna ukosefu wa uratibu kati ya wizara na idara nyingi za serikali ya Kenya zinazohusika na utekelezaji wa sheria hizi.
Nchi ya Kenya ina sheria nyingi za kazi, zingine hazitumiki moja kwa moja katika usafirishaji wa wafanyakazi nje ya nchi na hivyo kuzifanya zisifae usalama wa wafanyakazi wahamaji. Wizara ya kazi, wizara ya mambo ya nje na mambo ya ndani za Kenya na idara zingine kadhaa, halmashauri na bodi za ufadhili zote zinahusika katika kudhibiti usafirishaji wa wafanyikazi nje ya nchi. Lakini kukosekana kwa uratibu kati ya mashirika haya mengi kunadhoofisha utekelezaji wa sheria. Upungufu huu unazuia uwezo wa kuhakikisha ustawi na ulinzi wa waathirika wa biashara haramu kutoka kwa soko la uhalifu lililopangwa vizuri.
Mfumo thabiti wa udhibiti na utekelezaji ulio na sera moja kamili ya ajira ya kigeni unahitajika ili kusimamia usafirishaji wa wafanyakazi nje ya nchi na pia kushughulikia mitandao inayohusika na biashara haramu.
Sheria ya Kenya Dhidi ya Biashara Haramu ya Watu inasema kwamba biashara haramu ni wakati mtu 'anamsafirisha, anamhamisha, anamhifadhi au kumpokea mtu mwingine kwa madhumuni ya unyanyasaji'. Sheria hii inaeleza unyanyasaji kama unaojumuisha kumweka mtu katika hali ya utumwa na kumlazimisha kufanya kazi akiwa ameridhia au bila idhini ya mtu huyo. Licha ya sheria hii kutumika kwa karibu miaka 10 na kuwa na adhabu kali ya kati ya miaka mitano jela hadi kifungo cha maisha, haijazuia uhalifu huo.
Ofisi ya Kenya ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma inaripoti hivi sasa kushughulikia kesi 30 za biashara haramu ya binadamu. Lakini hakuna faili yoyote inahusu kazi ya kulazimishwa katika nchi za Mashariki ya Kati. Hii inaonyesha kuwa biashara haramu ya binadamu kwenda Mashariki ya Kati haijatambuliwa au haijapewa kipaumbele na serikali.
Lucia Nekesa, aliyeajiriwa kama mfanyakazi wa nyumbani kwenda Qatar na shirika la ajira nchini Kenya, alijikuta yuko Iraq iliyoharibiwa na vita. Kupitia video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii mnamo Agosti 2019, Nekesa anaeleza kwamba alidhulumiwa na kutumiwa katika biashara hii haramu mara sita katika muda wa miezi 10.
Aliokolewa na serikali ya Kenya kwa msaada wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji na HAKI Afrika - shirika la kiraia la Kenya - mnamo Septemba 2019. Mathias Shipeta, afisa wa mwitikio wa haraka wa HAKI Afrika, anasema kuwa ni nadra kwa waathiriwa wa biashara haramu ya wanadamu kuokolewa - akisema kwamba kesi ya Nekesa ilikuwa ya kipekee.
ENACT walifanya uchunguzi mnamo Mei 2019 katika maeneo ya mashariki ya Kenya, pwani na Nairobi uliohusisha wafanyakazi waliorejea ambao walikuwa wamehamishwa kupitia biashara haramu na familia za wahasiriwa ambao bado walikuwa na jamaa katika nchi za Mashariki ya Kati.
Utafiti uligundua kuwa karibu wafanyakazi wote 60 waliohojiwa walidhulumiwa mahali pao pa kazi. Hii ilihusisha unyanyasaji wa kimwili na kutukanwa, vitisho na kutishwa, kukatazwa matibabu, saa nyingi za kufanya kazi, kudhibiti wanakokwenda na mawasiliano yao, unyanyasaji wa kijinsia kazini, kupatiwa chakula duni na kuishi na kulala katika vyumba visivyostahili.
Karibu wote walibadilishiwa masharti ya mikataba yao ya ajira walipofika katika nchi walizokusudia. Haya yalijumuisha kupunguzwa kwa mshahara, mabadiliko ya eneo la kazi na saa nyingi za kufanya kazi.
Mnamo Septemba 2014 serikali ya Kenya ilipiga marufuku mashirika ya ajira kuwaajiri Wakenya kufanya kazi katika nchi za nje kwa sababu ya malalamiko yaliyotolewa na waathiriwa waliouzwa nje ya nchi, wafanyakazi waliorejea, vyama vya wafanyakazi na mashirika ya asasi za kiraia. Hii ilisababisha kuanzishwa kwa jopo kazi la mashirika mengi mnamo Oktoba 2014 ambalo lilikuwa na lengo la kutoa mapendekezo ya kulinda wafanyakazi wahamiaji na kudhibiti shughuli za ‘mashirika ya ajira yasiyo na ofisi maalum'.
Jopo kazi hili liliripoti kwamba karibu Wakenya 200,000 walikuwa wanafanya kazi katika nchi za Mashariki ya Kati, na kati yao 130,000 walikuwa Saudi Arabia na 22,000 katika Milki za Kiarabu. Nchi zingine ni Qatar, Oman, Bahrain, Jordan, Lebanon, Yemen na Iraq.
Mapendekezo kumi na saba yalitolewa - ambayo ama yametekelezwa kwa sehemu tu au hayajatekelezwa kabisa. Jopo kazi pia halikufanya mapendekezo kuhusu mchakato wa kuyachunguza na kuyahukumu mashirika ya ajira ya kigeni na ya ndani yanayowauza Wakenya kwa sasa.
Pia hakuna chochote kuhusu namna ya kushughulikia wafanyakazi ambao walisafirishwa kabla ya marufuku na ambao bado wanauzwa katika nchi za nje. Inaonekana kuzingatia zaidi unyanyasaji ambao Wakenya wanakabiliwa nao mara tu wanapowasili katika nchi za nje badala ya mchakato waliopitia hapo awali.
Licha ya serikali kuweka mchakato mpya wa usajili wa mashirika ya ajira mnamo 2017, biashara haramu inaendelea kuchangia uchumi wa kiuhalifu wa chini kwa chini wa Kenya. Uchunguzi wa ENACT uliofanyiwa mashirika 20 ya ajira nchini Kenya ulibainisha aina mbili za wahusika wa uhalifu wanaoendesha soko hili.
Kwanza ni mitandao ya jinai ya kigeni ya mataifa mbalimbali inayohusika katika biashara haramu ya wanadamu kwa kisingizio cha kuwaajiri watu. Imepangwa vizuri sana na ina muundo wa kimlalo wa kufanya kazi unaoonyesha kuwa viungo mbalimbali kwenye msururu wa matukio hufanya kazi kivyao, lakini vyote vinashirikiana na mitandao ya jinai iliyopangwa ya eneo husika kwa kujifanya kuwa mashirika ya ajira.
Pili ni mitandao ya uhalifu ya eneo husika. Mashirika ya ajira ya eneo husika, hasa yale ambayo hayana kibali, yana mpangilio wa hali ya juu, yakiwa na muundo wima wa kufanya kazi unaoonyesha kuwa mbinu za shughuli za vikundi tofauti hufanya kazi pamoja vikiwa na mpangilio wazi wa utoaji amri. Wajasiriamali hawa wako nchini Kenya na hufanya kazi na mashirika ya ajira ya kigeni yanayohusika na biashara haramu.
Serikali ya Kenya na wadau wengine wamelishughulikia suala hilo kama suala la haki za binadamu badala ya kosa la jinai. Hata katika mfumo wa msingi wa haki za binadamu ulio na lengo la kuwalinda wafanyakazi, uingiliaji kati hadi sasa haujatosha na mwelekeo wa kipekee wa kuzingatia haki umechepua umakini kutoka kwa mwelekeo wa jinai. Kuliangalia tena tatizo hili kama biashara haramu ya binadamu kungesaidia Kenya kuwalinda wafanyakazi wake nje ya nchi wakati wa kupambana na uhalifu wa kimataifa.
Uhamaji huchangia 3% ya wafanyakazi wote ulimwenguni na umekuwa mojawapo ya sehemu muhimu za uchumi wa dunia. Hali ya jinsi nchi zinaweza kusaidia uhamiaji wa wafanyakazi kama rasilimali ya mabadiliko ya maendeleo ina mashiko.
Mabadiliko katika uchumi wa dunia na teknolojia inayoendelea yanapunguza faida ya kuwa na akiba ya wafanyakazi wasio ghali. Kwa hivyo, Kenya inapaswa kukuza mkakati wa muda mrefu wa kuleta utulivu katika uwezo wa mapato ya nje ya nchi.
Mohamed Daghar, Mtafiti, Mradi wa ENACT, ISS