Wanawake tisini na sita kutoka Uganda, wengi wao wakiwa watoto na vijana, walisimamishwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Nairobi katika mwezi wa Januari wakiwa njiani kuelekea Milki za Kiarabu (UAE) kutafuta kazi. Wasichana hao, ambao hawakuwa na nyaraka sahihi za ajira, walikuwa waathiriwa wa kundi la biashara haramu ya binadamu huko Afrika Mashariki, lenye makao makuu yake nchini Kenya na linaloendesha shughuli zake likisingizia kuwa mawakala wa ajira.
Hii haikuwa mara ya kwanza kukamatwa. Karibu kila mwezi, Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Kenya huripoti angalau kisa kimoja cha kukamatwa kwa waathiriwa sio tu kutoka Uganda lakini pia Burundi, Rwanda na kwa kiwango kidogo Tanzania. Biashara nyingi ya usafirishaji haramu wa binadamu ya Afrika Mashariki hufanyika nchini Kenya au hupitia humo.
Kijadi, mkufu wa thamani wa mtandao huu wa uhalifu umejumuisha viungo vitatu. Kwanza, ni madalali wa ajira wa ukanda ambao husafirisha watu kutoka nchi zao hadi Kenya. Pili, ni viungo vya Kenya ambavyo 'hupokea' watu na hujifanya kama mawakala wa ajira wa nchi. Wao huhamisha waathiriwa kutoka Kenya hadi nchi pokezi. Tatu, ni wenzao ambao mara nyingi hujifanya kama mawakala wa ajira za kigeni. Hawa wanapatikana katika nchi pokezi na 'huwapokea' watu waliotumwa kutoka Kenya.
Kesi za hivi karibuni na utafiti mpya uliofanywa na mradi wa uhalifu uliopangwa wa ENACT unaonyesha kwamba kuna mabadiliko katika utendaji wa shughuli za biashara haramu hasa kuhusu 'kiungo' cha tatu. Kuna ushahidi kwamba biashara haramu ya kusafirisha wanawake na wasichana kutoka Afrika Mashariki kwenda Mashariki ya Kati hivi sasa inafanywa na wananchi wa Afrika Mashariki pekee.
Mahojiano yaliyofanywa na waathiriwa yalifichua kwamba walipokelewa katika nchi hiyo ya kigeni na 'watu wanaowafahamu'. Mnamo Februari 2020, Wakenya 50, ambao kila mmoja alilipa takriban Dola 2,000 za Marekani kwa waliodai kuwa mawakala wa ajira, walisafirishwa kwenda UAE na kutiwa utumwani katika nyumba na ‘wakala wa Mombasa’ ambaye anafanyia shughuli zake Mombasa na Dubai. Waathiriwa walisema kwamba kulikuwa na 'nyumba nyingi za biashara haramu' kama hii zinazoendeshwa na Wakenya huko Dubai, zinawahifadhi raia wengine wa Afrika Mashariki kama Waganda na Watanzania.
Kisa mahususi kilichofichuliwa kwa Lucia Bird, Mchanganuzi Mwandamizi katika Mpango wa Ulimwengu Dhidi ya Uhalifu Uliopangwa Unaovuka Mipaka ya Kitaifa, kinaonyesha mahusiano ya kimataifa na kikanda. Msichana Mganda alisafirishwa hadi Kenya na rafiki yao wa kifamilia ambaye pia ni Mganda. Kisha raia wa Kenya akasafiri naye kwa ndege hadi Oman ambapo alichukuliwa katika uwanja wa ndege na raia wa Ethiopia kabla ya kupelekwa kwa waajiri wake wa Omani.
Vivyo hivyo, Angelo Izama, mshauri wa biashara haramu ya binadamu ambaye hujitolea katika mradi wa waathiriwa wa biashara hiyo haramu katika kanisa huko UAE, aliiambia ENACT juu ya msichana Mganda aliyeajiriwa kuwa mpokea wageni. Alipokelewa na Mganda huko Dubai na kulazimishwa kufanya kazi ya ukahaba.
Huku viungo katika mkufu wa thamani wa jinai hufanya kazi pamoja, pia kuna ushindani, huku waendeshaji wakishindania mgao mkubwa wa vipengele vyenye faida zaidi kwenye shughuli hiyo. Mitandao ya biashara haramu ya kikanda inaonekana kutaka kudhibiti mkufu wote wa thamani, kuanzia kutafuta hadi kuwaajiri waathiriwa, kuwasafirisha nje ya Afrika Mashariki, na kuwapokea katika nchi ya kigeni. Mchakato huu wa uhalifu wa kimataifa ulioratibiwa vizuri na unaobadilika kila wakati ni mgumu kuzuiwa kwa kutumia polisi na kushtaki.
Akiongea kwa sharti la kutotajwa jina, afisa wa polisi ambaye ni mtaalamu wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu Afrika Mashariki aliiambia ENACT kuwa shida hiyo imeenea katika ukanda huo. Hii inathibitisha ripoti ya tathmini ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Mihadarati na Jinai (UNODC) ambayo inaonyesha ongezeko la biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu katika nchi za Afrika Mashariki.
Afisa huyo pia anabainisha kuwa kuzuia uhalifu huo kunazidi kuwa kugumu. Kama mfano, afisa huyo alirejelea juhudi za pamoja mnamo 2017 kati ya serikali za Kenya na Uganda ambazo zilionekana kutoa matumaini katika hatua zake za kupambana na biashara hii haramu. Hata hivyo, zilishindwa kwa sababu ya kukosekana kwa taarifa sahihi za kijasusi kuhusu mkufu wa thamani wa jinai, na ushirikiano usio na utaratibu kati ya nchi hizo mbili.
Kudhibiti sekta ya kupeleka wafanyikazi nje ya nchi pia ni suala changamano. Kama ilivyofanya Kenya, Uganda iliweka marufuku ya uhamiaji wa wafanyikazi hadi Mashariki ya Kati katika mwaka wa 2016, na kisha ikaiondoa mwaka mmoja baadaye. Mashirika ya kiraia ya Uganda yanayofanya kazi ya kukabiliana na biashara haramu ya binadamu yalisema kwamba marufuku hiyo na kuondolewa kwake vilikuwa na athari ndogo kwa shughuli nzima. Walihoji faida za kusafirisha wafanyikazi nje ya nchi na wakaangazia hali ya kutowalinda wale wanaoshughulikia uhamiaji wa wafanyikazi.
Mashirika ya kikanda kama kama vile Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, UNODC na Umoja wa Ulaya mara nyingi yameomba kuwepo na mkakati imara wa kikanda kuhusu biashara haramu. Mkakati wa hivi karibuni zaidi ni mpango wa Usimamizi Bora wa Uhamiaji ambao unatetea uzuiaji, ulinzi na ufunguliwaji mashtaka kwa wanaoshiriki katika biashara haramu ya kusafirisha binadamu katika eneo la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.
Nchi za Afrika Mashariki zinaonekana kukosa uwezo wa kushauriana na nchi za Mashariki ya Kati kuhusu maswala ya biashara haramu. Hii ni kwa sababu ya upungufu uliopo katika sheria zao za ndani na mikakati ya biashara haramu ya kikanda. Hata hivyo, kanda nyingine zinazopeleka wafanyikazi kule Mashariki ya Kati zimeonyesha kuwa hili linawezekana.
Kwa mfano, nchi ya Ufilipino ina mapatano 23 (yanayohusu nchi mbili) na nchi saba - nyingi zikiwa ziko Mashariki ya Kati. Hili linawezesha mamlaka kusimamia ulinzi na usalama wa wafanyikazi na kuwazuia kunyanyaswa na mitandao ya biashara haramu na waajiri katika nchi wanazoenda. Sekta ya biasharanje ya wafanyikazi ni sehemu muhimu sana ya pato la ndani la Ufilipino, lakini pia ina changamoto na sio tiba kamili ya kiuchumi.
Afrika Mashariki inahitaji kujifunza kutoka kwa njia zilizotumiwa kwingine ambazo zinazuia biashara haramu na kuwalinda wafanyikazi. Hadi pale ambapo mbinu imara zitakapotumiwa, biashara haramu na unyonyaji vitaongezeka katika ukanda huu. Hii inaendeleza hali ya wanawake na wasichana maskini kuweza kuathiriwa kwa urahisi na inadhoofisha matarajio ya usafirishaji wa wafanyikazi nje ya nchi kama njia ya kuchuma riziki.
Mohamed Daghar, Mtafiti, Mradi wa ENACT, ISS

