21 Jan 2020

Kuwalinda watoto walio katika hatari ya kudhuriwa zaidi nchini Kenya

Marufuku ya jumla ya taasisi za watoto za kutoa misaada sio njia ya kukomesha dhuluma dhidi ya watoto nchini Kenya.

Mfululizo wa uchunguzi wa vyombo vya habari unahusisha taasisi za watoto za kutoa misaada (CCI) na biashara haramu ya watoto na mitandao ya kulazimishwa kuomba nchini Kenya na inayohusisha Uganda na Tanzania katika ukanda huu.

CCI ni vituo vya kibinafsi vinavyodhibitiwa na serikali. Vituo hivi hujumuisha vituo vya watoto yatima na vituo vya ulemavu na ulinzi wa watoto walio katika hatari ya  kudhuriwa zaidi. Theluthi moja ya waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu duniani ni watoto. Nchini Kenya, takribani 20% ya waathiriwa wa biashara haramu ni watoto wenye umri chini ya miaka 18. Dhulumu dhidi ya watoto ni uhalifu na hasa inapofanywa kwa sababu ya faida.

Asilimia arubaini na moja ya watoto wote wanaouzwa Afrika Mashariki huingizwa katika biashara hii haramu kupitia kwa familia zao, na watoto wengi katika CCI wana familia ambazo ziliwaweka hapo. Hii ni kwa sababu familia zinaamini kwamba watoto wao wanaweza kupata elimu na chakula na kuwa salama. Familia zingine hulipa CCI ada ndogo ili iwachukue watoto wao.

Michelle Oliel, mwanzilishi mwenza wa shirika lisilo la faida la Stahili Foundation linalofanya kazi ya kuwalinda watoto, ameambia ENACT kuwa CCI, hasa katika kaunti zilizo kwenye mpaka wa Kenya na Uganda na Tanzania, zinahusika na biashara haramu. CCI hizi huendeshwa kama vituo vya watoto yatima au walemavu na huwachukua  watoto kuomba mitaani. Miji iliyo mpakani nchini Kenya ni maeneo yenye shughuli nyingi za kibiashara zinazovuka mipaka hadi Uganda na Tanzania.

Mfululizo wa uchunguzi wa vyombo vya habari unahusisha taasisi za watoto za kutoa misaada (CCI) na biashara haramu ya watoto na mitandao ya kulazimishwa kuomba, nchini Kenya, Uganda na Tanzania

Watoto, hususan walemavu, huwekwa katika maeneo muhimu katika mitaa husika ya mipaka wa Kenya na Uganda na Tanzania ili kuomba. Kila kundi la watoto lina msimamizi anayewaelekeza wamfuate nani na kuomba pesa. Msimamizi hukusanya pesa mara tatu hadi nne kwa siku kutoka maeneo haya. Haijulikani pesa hizi hutumika kufanya nini, lakini mbali na faida za kibinafsi, fedha huhamishwa  kwa urahisi kwa sababu sarafu za nchi zote mbili zinakubaliwa kwa kiasi kikubwa katika kaunti za mipaka ya Kenya.

Aina nyingine ya kulazimishwa kuomba hufanyika katika CCI zinazofanya kazi katika maeneo ya miji ya Kenya na hufanyika kwa njia nyingi. Kuna 'safari za kutembelea vituo vya watoto yatima' ambazo zinatoa 'mpango wa jumla' kwa wageni ambao wanataka kutembelea na kuwa wafanyakazi wa kujitolea kwenye CCI. Viwango vya mpango huu wa jumla ni vya juu, kuanzia Dola za Kimarekani 3 000 kwa wiki bila kujumuisha gharama za usafiri wa ndege na visa. Pesa nyingi zinazokusanywa haziboreshi hali mbaya ya baadhi ya CCI. Oliel anasema kuwa watu ambao husimamia CCI wanaishi maisha mazuri katika maeneo ya kifahari katika miji yao.

Leah Wambui, kijana na mkazi wa zamani wa CCI jijini Nairobi, anaambia ENACT kwamba alipokuwa huko, watoto walilazimishwa kuimba na kujifanya 'wanyenyekevu' ili kuvutia huruma kila wakati wageni kutoka nje ya nchi walipokuja. Walikatazwa kuzungumza waziwazi na watalii wa nje au watu wa kujitolea. Wambui alishambuliwa na viongozi wa CCI kwa kuwajulisha wafanyakazi  wa kujitolea kuwa ustawi wao haukushughulikiwa na kwamba walizuiliwa na hawakuwa na uhuru wa kutembea.

Theluthi moja ya waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu duniani ni watoto. Nchini Kenya, takribani 20% ya waathiriwa wa biashara haramu ni watoto wenye umri chini ya miaka 18

CCI ni vituo vya utunzaji wa kitaasisi vya muda na ni kimbilio la mwisho kwa watoto. Matarajio ya serikali ni kwamba mtoto asiwekwe katika CCI kwa zaidi ya miaka mitatu,na baada ya hapo mahali pa kudumu panatakiwa kupatikana. Lakini kwa sababu kuna faida kubwa katika kuendesha hizi CCI, ukitumia watoto waliozuiwa pale kama chambo, watoto wengi hukaa pale kwa muda mrefu.

Pia serikali haitofautishi kati ya watoto ambao walisafirishwa (hasa kutoka nje ya nchi) na watoto wa Kenya ambao wamewekwa huko na familia zisizojiweza au ni yatima.

Serikali ya Kenya ilianzisha mchakato wa kuzibadilisha CCI kwa kuanzisha mwongozo wa utunzaji mbadala wa watoto unaofanywa na familia. Mwongozo huu unaongozwa na sheria kadhaa za watoto nchini Kenya kama kanuni za CCI, 2005, na kimataifa kama vile Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Watoto, 1990. Mwongozo huu ulipelekea kuwepo kwa mpango wa utekelezaji wa 2015-2022 wa watoto nchini Kenya.

Jambo muhimu katika mabadiliko hayo lilikuwa agizo la 2017 la kusitisha kwa muda usajili wa CCI mpya. Hii ni hatua nzuri ambayo ilisababisha zoezi la kutambua CCI zilizopo na mahali zilipo. Kuna pengo la data kuhusu idadi ya watoto walio kwenye CCI. Serikali ya Kenya na Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa ziliripoti kwamba watoto 42 000 walirekodiwa kuishi katika CCI zaidi ya 700, baadhi ambazo hazijasajiliwa kisheria. Wataalamu wanaeleza kwamba huku ni kutosema ukweli wote.

Asilimia arubaini na moja ya watoto wote wanaouzwa Afrika Mashariki huingizwa katika biashara hii haramu kupitia familia zao

Marufuku ya serikali kwa taasisi hizi zote inaweza kuwa na athari mbaya kwa kazi nzuri ambayo baadhi ya CCI zinafanya katika kutoa makazi na kutoa mazingira kama ya familia kwa watoto, tukizingatia idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika CCI.

Hakuna data kamili kuhusu idadi ya watoto walio kwenye CCI. Hii imekuwa mojawapo ya mambo ambayo yamezuia uingiliaji kati katika kushughulikia biashara haramu katika taasisi hizi. Kwa sababu ya wito kutoka kwa wataalamu wa ulinzi wa watoto kupiga marufuku CCI zote kufanya kazi, serikali inahusika katika mradi wa majaribio na kaunti tano kukusanya data ya idadi ya watoto walio katika CCI. Vyanzo vinavyohusika katika mradi huo pia vinathibitisha kwamba baadhi ya CCI hizi zinahusika katika biashara haramu ya watoto na nyingine hazijasajiliwa vyema au hazijasajiliwa kabisa.

Data kutoka mradi huu itasaidia serikali na wadau wengine wa ulinzi wa watoto kama Mashirika Yasiyo ya Serikali (NGO), vikundi vya utetezi wa haki za watoto na CCI ili kuunda mikakati ya kushughulikia biashara haramu ya watoto katika CCI za Kenya. Data hii inaweza pia kuongoza juhudi za kieneo zinazohusisha Kenya, Uganda na Tanzania katika kusaidia kushughulikia tatizo la biashara haramu ya watoto inayovuka mipaka.

EU Flag
ENACT is funded by the European Union
ISS Donors
Interpol
Global
ENACT is implemented by the Institute for Security Studies in partnership with
INTERPOL and the Global Initiative against Transnational Organized Crime.