Uamuzi wa Kenya wa kuondoa mashirika ya serikali, ikiwa ni pamoja na wakaguzi wa kitabibu, kutoka Bandari ya Mombasa kunaweza kuhatarisha afya ya Wakenya na raia wa nchi jirani zisizokuwa na bandari.
Rais Uhuru Kenyatta aliondoa utaratibu ulioimarishwa ulioanza kutumika miezi miwili iliyopita ili kupunguza uingizaji kwa wingi wa dawa bandia nchini. Mwaka uliopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa tahadhari juu ya Augmentin bandia iliyopatikana nchini Kenya na Uganda - onyo lake la pili kuhusu ugunduzi wa dawa bandia za antibiotiki barani Afrika.
Hadi agizo la Kenyatta kutolewa, Bodi ya Dawa na Sumu ya Kenya (PPB), Mamlaka ya Dawa ya Taifa ya Uganda (NDA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Rwanda zilifanya kazi kwa pamoja kukagua dawa katika Bandari ya Mombasa, bandari moja inayotumiwa kuingia katika nchi hizo tatu. Pia walifanya ukaguzi wa kila furushi la bidhaa za dawa na kutambua wafanyabiashara waliotiliwa shaka ambao walifanyiwa ukaguzi mkali zaidi.
Ushirikiano huo wenye nguvu sasa haupo tena. Mashirika ya serikali ambayo hapo awali yalipewa jukumu la kukagua mizigo iliyoingizwa katika bandari yalipunguzwa kutoka 30 hadi matatu. Kusudi la kimsingi la upunguzaji huu ilikuwa ni kuharakisha uidhinishaji wa shehena kuchukuliwa. Sasa mizigo mingi hukaguliwa katika bandari ya asili kwa bidhaa zinazopelekwa nje, ikiwa ni pamoja na bidhaa za dawa.
Tahadhari ya kwanza ya WHO ilitolewa mnamo 2018 baada ya dawa bandia kupatikana katika masoko ya mitaani ya Douala, Kameruni. WHO ilieleza kwamba 'Ufungaji wa bidhaa bandia unaonekana kuiga kwa karibu bidhaa halisi zinazotengenezwa na GSK (GlaxoSmithKline).’ Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, GSK ilikataa furushi hilo la dawa bandia.
WHO ilihusisha tahadhari hiyo na taarifa za kijasusi kutoka NDA ya Uganda na PPB ya Kenya. Hii ilitokana na uchunguzi wa mara kwa mara wa baada ya bidhaa kuingia sokoni kuhusu ubora wa bidhaa za matibabu. Afisa Mkuu Mtendaji wa PPB Dkt. Fred Siyoi alisema katika kongamano la vyombo vya habari jijini Nairobi muda mfupi baada ya tahadhari kutolewa kwamba taasisi hizo mbili za kitaifa zilipeleka habari hizo kwa mfumo wa tahadhari wa haraka wa WHO na INTERPOL.
Wadau wa viwanda vya dawa vya Kenya wanaamini kwamba uangalifu kama huo unaweza kuathiriwa na uamuzi wa Kenyatta na kusababisha ongezeko la visa vya dawa bandia zinazoingia nchini. Waingizaji bidhaa wasioidhinishwa, ambao dawa zao zilizoingizwa nchini kwa udanganyifu waliosimamishwa hapo awali, huenda walitumia kwa manufaa yao kule kutokuwepo kwa PPB kwenye bandari. Waliambia mradi wa ENACT unaoshughulikia masuala ya uhalifu uliopangwa kwamba walikuwa wametuma malalamishi dhidi ya agizo la rais kwa maslahi ya afya ya umma.
Hata hivyo, si kila mtu anakubali kwamba amri hiyo itasababisha kuongezeka kwa dawa bandia katika eneo hili. Kulingana na PPB, 99% ya dawa nchini kwa sasa zina ubora unaostahili. 'Hakuna dawa ghushi nchini Kenya; 1% tu ndiyo inaweza kuchukuliwa kuwa na ubora duni,‘ Dkt. Ronald Inyangala, mkurugenzi wa PPB anayesimamia biashara, aliiambia ENACT.
Hata hivyo, Dkt. Anastasia Nyalita, mwenyekiti wa Chama cha Viwanda vya Dawa Nchini Kenya, aliambia ENACT kwamba 'chapa zilizoimarika tu ndizo zinaripotiwa ikiwa kuna shida yoyote. Zile zinazohusiana na bidhaa ghushi zinazouzwa katika maduka ya dawa ambayo hayana leseni huwa haziripotiwi kwa hofu ya kusababisha msukosuko sokoni. '
Nchini Uganda, NDA inakiri kuwa asilimia 10 ya dawa zilizo nchini humo ni za kiwango cha chini au ni dawa bandia ambazo zimeuzwa madukani. Mwenyekiti wa Bodi ya NDA Dkt Medard Bitekyerezo aliliambia gazeti moja Nchini Uganda kwamba 'bidhaa bandia huingia nchini kupitia mipaka isiyodhibitiwa, kupitia Ziwa Victoria.’ Gazeti hili linasema kuwa nchini jirani za Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaaminika kuwa ndio asili ya dawa bandia.
Watu wengi wasioshiriki moja kwa moja wanaamini kuwa dawa bandia ni shida inayoongezeka katika eneo hili. Hii ni kwa sababu ya uwepo wa kile ambacho wadau wanaita waingizaji bidhaa nchini 'wasiodhibitiwa' au 'wasio na ofisi' ambao aghalabu hutumia mizigo iliyounganishwa. Kuna uwezekano wa waingizaji bidhaa kutoka nchi za nje kama hao kuongezeka kutokana na gharama kubwa ya kufanya biashara katika nchi za eneo hili zenye uchumi mdogo.
Imesemekana kwamba 'kikundi shawishi chenye nguvu' nchini Kenya kikiongozwa na Chama cha ya Waingizaji Bidhaa kutoka Nje na Wafanyabiashara Wadogo ndicho kilisababisha kutolewa kwa agizo la Kenyatta. Kikundi hiki cha ushawishi kinalalamika kwamba mashirika mengi katika bandari huchelewesha kutolewa kwa idhini ya kuchukua mizigo yao iliyotoka nje ya nchi katika vyombo vilivyojumuishwa. 'Hiki [kikundi shawishi] kinapinga kuwepo kwa uthibitishaji kamili wa kubainisha utangazaji makosa wa mali na ughushi,' afisa wa KPA aliyekataa kutajwa aliiambia ENACT.
Wadau wanatilia shaka uwezo wa mashirika matatu ya serikali yaliyopewa jukumu la kufanya ukaguzi wa siku za usoni. Mashirika haya ni Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) ambayo inasimamia bandari, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini Kenya (KRA) na Shirika la Ukadiriaji Ubora wa Bidhaa Nchini Kenya ( KEBS).
'KEBS haina uwezo wa kufanya uchanganuzi wa ukaguzi wa bidhaa za dawa na kuhakikisha kuwa kampuni zinatii sheria na taratibu zilizowekwa,' Nyalita alisema. Alieleza kuwa wauzaji bidhaa nje sasa wamelazimika kutumia maabara ya nje na kupitisha gharama hiyo ya ziada kwa watumiaji. Hili linaongeza gharama ya dawa zilizoingizwa nchini kihalali. Linaongeza muda wa mchakato wa ukaguzi, hali inayofupisha kwa hadi 75% ya maisha ya bidhaa kutumika zinazofikia soko la kawaida.
Ripoti ya hivi karibuni ya Mkaguzi Mkuu wa fedha za serikali inaonyesha kwamba Shirika la Usambazaji wa Dawa Nchini Kenya lilikuwa kufikia mwisho wa mwaka 2018 limetoa dawa ambazo muda wake wa kutumika umeisha zenye thamani ya Dola milioni 1.50 kwa hospitali za serikali za eneo hilo. Hatari ya dawa ambazo muda wake wa kutumika umekwisha na gharama ya juu ya bidhaa halali za dawa hufanya dawa za kiwango cha chini kuwa chaguo rahisi.
WHO inahitaji serikali zianzishe mamlaka imara za udhibiti wa dawa za kitaifa. Mamlaka hizi zinapaswa kuwa na dhamira iliyo wazi na msingi mzuri wa kisheria, kiufundi na kifedha. Zaidi ya yote zinapaswa kuwa na uwezo wa kushinikiza udhibiti ufaao wa soko pamoja na ufuatiliaji na tathmini inayofaa. Mamlaka zinapaswa kuwa na uwazi na uwajibikaji kwa serikali na umma.
Kuishiwa dawa katika hifadhi ya kitaifa na gharama ya juu ya bidhaa bora kunaweza kusababisha athari mbaya na hatari Afrika Mashariki yote-. Sera zinazofanywa kwa haraka bila kutathminiwa zinaweza kuzidisha hali hii. Badala yake, maamuzi yanayoathiri usambazaji na mahitaji kuhusu bidhaa nyeti za dawa yanapaswa kufanywa na mamlaka za kisheria ili kuzuia ueneaji wa dawa bandia, chanjo na bidhaa za kibayolojia bandia.
Deo Gumba, Mratibu wa Kieneo wa Kituo cha Kuchunguza Uhalifu Uliopangwa - Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, ISS
